Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo imetangaza orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 47­,305 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 150.03 bilioni kwa mwaka wa masomo 2020/2021 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.

Akitangaza orodha hiyo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao (47,305), wanaume ni 26,964 sawa na asilimia 57.37 na wanawake ni 20,341, sawa na asilimia 42.63.

Aidha, Badru amesema HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru katika mkutano uliofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam.

Tarehe ya kutolewa orodha ya Awamu ya Pili

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Pili, Badru amesema imepangwa kutolewa Jumamosi, Novemba 14, 2020 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao za SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Wanafunzi hawa wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mkopo kwa kuwa wana sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja. Tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili katika siku mbili zijazo, yaani Jumamosi, Novemba 14,” amesema Badru.

Upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa pili na kuendelea

Aidha, katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa wanafunzi wote ambao wana mikopo wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wapatao 44,629 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 155.06 bilioni.

“Wanafunzi hawa 44,629 wamepangiwa mikopo baada ya HESLB kupokea matokeo ya mitihani yanayothibitisha kuwa mwanafunzi amefaulu kuendelea na masomo katika mwaka unaoanza,” amesema Bw. Badru na kufafanua HESLB inaendelea kupokea matokeo ya wanafunzi waliokua na mikopo mwaka wa masomo uliopita na watapangiwa mikopo.

TZS 464 Bilioni zimetengwa kwa mikopo ya elimu ya juu 2020/2021

Katika mkutano huo, Bw. Badru ameeleza kuwa Serikali imetenga TZS 464 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 145,000. Kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na 91,000 ni wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka.

Wito

Aidha, Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Imetolewa na:

BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

DAR ES SALAAM

Jumatano, Novemba 11, 2020