TAMKO LA JUKWAA LA ELIMU KWA MTOTO WA KIKE KUHUSU KAULI YA MH. HALIMA DENDEGO MKUU WA MKOA WA SINGIDA.
Utangulizi
Elimu ni haki ya kila mtoto nchini Tanzania, ni nguzo ya kupambana na umaskini, na ni nyenzo ya kuwawezesha watoto kufikia ndoto, kubadili fikra na kutatua changamoto zao na jamii. Serikali na wadau mbalimbali wameweka nguvu katika kuboresha mifumo ya elimu, ili kurahisisha upatikanaji wa elimu sawa kwa wote kama ilivyoanishwa kwenye ibara ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977.
Sisi, kama mashirika yanayounda jukwaa la elimu kwa mtoto wa kike, tumesikitishwa na kauli iliyotolewa na Mh. Halima Dendego, Mkuu wa Mkoa wa Singida, mnamo tarehe 21 mwezi Aprili 2024, katika ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya wilaya ya Itigi alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Kitaraka. Tuna nukuu;
“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshitakiwa namba Moja na wewe ndio utakayeenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko kwa sababu mna tabia ya ukipata mimba tunaenda kukimbizana na mtoto wa kiume si sawa wote mlishirikiana kwa hiyo yeye atakuwa mshitakiwa namba mbili na msichana atakuwa mshitakiwa namba Moja”.
Aliendelea kwa kuagiza wanafunzi wa kike waliopata mimba wakiwa shuleni kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria pamoja na wazazi wao.
Kauli ya Mh. Dendego, inasahau chanzo cha mimba za utotoni katika jamii yetu na kuwahukumu wasichana kama ndio chanzo na suluhu pekee ya kumaliza tatizo la mimba za utotoni. Kauli hii inarudisha nyuma jitihada zinazochukuliwa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa elimu katika kuhakikisha tunaondoa vikwazo na kila mtoto anapata fursa ya kupata haki ya elimu.

Kwa taaarifa zaidi tafadhali pakua tamko lote hapa.