Kwa muda mrefu kumekuwa na matukio mablimbali ya athari ya viboko kwa wanafunzi mashuleni kama vile kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu hadi vifo. Mtandao wa Elimu Tanzania unasikitishwa sana na matukio kama hayo hususani kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kinachosemekana kutokana na adhabu ya viboko aliyopata shuleni.

Ni adhma ya mzazi/mlezi kumpatia fursa ya kusoma mtoto wake na ni wajibu wa mwalimu kutimiza wajibu wake kwa uadilifu wa kumpatia elimu stahiki, kumtunza, kumlea na kumuongoza kwa kumkuza na kumwendeleza kimwili, kiakili na kiroho. Ni dhahiri kwamba si kusudio la mwalimu kumdhuru mwanafunzi kwa kumuadhibu bali kumjenga na kumrekebisha kwani mwalimu ni mlezi wa mwanafunzi shuleni.

Hivyo basi Mtandao wa Elimu Tanzania unapenda kuwakumbusha walimu wote nchini na wananchi kwa ujumla kuwa, mwongozo wa kutoa adhabu mashuleni chini ya kifungu cha 61 (1) (v) cha Sheria ya Elimu sura ya 353 marejeo ya mwaka 2002 ambao unampa mamlaka Waziri wa Elimu kutunga kanuni za Masuala mbalimbali zitakazokidhi utekelezaji wa masuala ya Sheria hiyo.

Miongoni mwa kanuni zilizotungwa ni pamoja na The Education (Corporal Punishment) Regulation G. N. 294 ya mwaka 2002. Kanuni hizi zinatoa mwongozo ni wakati gani adhabu ya viboko inatakiwa kutolewa na kwa kiwango gani.

Kanuni ya 3 (1) inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya Viboko itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne (4) kwa tukio lolote.

Sheria imempa mwalimu mkuu wa shule husika mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo. Mwalimu anayechaguliwa kutoa adhabu atakua na mamlaka ya kutoa adhabu pale tu atakapopata idhini ya mwalimu mkuu katika tukio husika

Kanuni ya (5) inataka kila adhabu ya kiboko inayotolewa kwa mwanafunzi kumbukumbu ya kutolewa kwa adhabu hiyo sharti iwekwe kwenye kitabu, ikitaja jina la mwanafunzi, kosa alilolifanya, idadi ya viboko na jina la mwalimu aliyetoa adhabu na kumbukumbu hizo lazima zisainiwe na Mkuu wa shule

Ni ukweli usiojificha kwamba, mwongozo wa adhabu hii tajwa hapo juu hutekelezwa kinyume cha kanuni zilizowekwa aidha kwa kutokujua au kwa kujua ila kwa kupuuzia. Ni vyema tukarejea kwenye kanuni zinazotuongoza kwenye utendaji kazi wetu wa kila siku na kuhakikisha walimu na wazazi wanauwelewa vya kutosha na kutekeleza kanuni ya utoaji adhabu ya viboko mashuleni

Mtandao wa Elimu Tanzania unapendekeza mambo yafuatayo:

  • Juhudi zaidi ziongezwe katika kuhamasisha utetezi wa vitendo vyote vya kikatili vinavyofanywa kwa mtoto na kuviweka hadharani ili sheria ipate kuchukua mkondo wake.

  • Serikali na mashirika mbalimbali yatoe elimu kwa walimu na wazazi kuhusu kanuni ya viboko mashuleni na utoaji wa adhabu mbadala kwa watoto .

  • Vyombo vya habari vizidi kujikita zaidi kwenye habari za uchunguzi na kuibua vitendo vyote vya ukatili na kuhabarisha umma juu ya namna bora za kumlinda mtoto.

  • Kila mwananchi atambue kwanza ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mmoja wetu bila kuangalia wadhifa, jinsia, kabila, dini au mahali.Mafunzo kwa waalimu juu ya malezi ya watoto na utoaji wa adhabu mbadala

  • Mwongozo wa utoaji wa adhabu ya viboko shuleni usambazwe shule zote na kila mwalimu apate nakala.

  • Walimu wakumbushwe mara kwa mara kuwa wana wajibu wa kumlinda mwanafunzi anakuwa shuleni na nje ya shule.

  • Kuwe na Kamati ya ulinzi wa mtoto shuleni

Mtoto ana haki ya kulindwa, kuendelezwa, kuishi, kushirikishwa na kutobaguliwa, tunatoka wito kwa wadau wote wa watoto tushirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha mtoto anapata haki zake na anafahamu wajibu wake.

Mtandao wa Elimu Tanzania ni mtandao unaowakilisha asasi za kiraia zisizopungua 181 zinazozijishughulisha na masuala ya elimu.

Bi Cathleen Sekwao

Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET)

To download the PDF Version of the press release click the link below:

TamkoJuuYaAthariZaAdhabuZaVibokoShuleni