Tamko Dhidi ya Udhalilishaji wa Watoto
Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ni mtandao unaoundwa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yapatayo 181 yanayojishughulisha na elimu Tanzania bara. Mtandao wa elimu unasikitishwa na kuendelea kwa vitendo visivyo vya kimaadili vya kuwarekodi wanafunzi na kisha kusambaza kwenye mitandao ya kijamii. Hayo hutokea katika hatua za kujifunza na walimu au wahusika hutumia udhaifu wa wanafunzi hao katika kujifunza kama jambo la kufurahisha jamii pasipo kujua ni kwa namna gani wanamdhalilisha na kumfedhehesha mwanafunzi.
TEN/MET inalaani na kukemea kwa nguvu vitendo vyote vinavyovunja au kwenda kinyume na taratibu za utoaji wa Elimu bora.
Ni wajibu wetu sote kutambua sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inatamka wazi kuwa, “Mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, au adhabu ya kikatili, kinyama au afanyiwe matendo yenye kumshushia hadhi”. Ni dhahiri kwamba, vitendo hivi si vya kufumbiwa macho bali ni vya kukemewa kwa nguvu zetu zote.
TEN/MET inatoa rai kwa walimu na watoa huduma katika mazingira ya shule na jamii kwa ujumla, kuacha mara moja kurekodi wanafunzi au watoto bila idhini ya mzazi au mlezi. Tunatoa rai pia kwa vyombo vya habari kuelimisha jamii juu ya madhara ya usambazaji wa maudhui hayo. Tunaomba serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kuzuia maudhui yoyote yanayoonyesha udhalilishaji kwa watoto na atakayekiuka achukuliwe hatua za kisheria.
NI WAJIBU WETU SOTE KUMTUMZA, KUMLINDA NA KUMWENDELEZA MTOTO,
Mr. Ochola Wayoga
Mratibu Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET)
Kupata nakala ya tamko hili bonyeza hapa chini:
Tamko dhidi ya udhalilishaji wa watoto