UTANGULIZI

Tanzania Education Network/ Mtandao wa Elimu Tanzania ni mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya miambili na kumi (210) yanayo fanya kazi Tanzania bara katika kanda kuu nane. Lengo la mtandao ni kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata haki yake ya msingi ya elimumsingi(basic education) iliyo bora. Kupitia wanachama tunaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha elimu itolewayo kuanzia chekechea hadi kidato cha IV ipo kwenye kiwango bora na itamjengea uwezo mtoto wa Kitanzania kupambana kimaisha. Mtandao unaipongeza serikali kwa kuendeleea kuwekeza katika elimu kwa kiasi fulani nchi imeweza kufanikisha utoaji wa elimu kwa wote.

CHANGAMOTO YA COVID-19 TANZANIA

Kama ilivyoelezwa na Wizara ya Afya mnamo tarehe 16 mwezi March 2020 iliripotiwa Tanzania kuwa na mgonjwa mwenye virusi vya corona, hivyo basi serikali ikachukua hatua ya kufunga shule na vyuo vyoye Tanzania ili kuhakikisha afya ya mtoto na mwanafunzi inachukuliwa kwa kipaumbele cha hali ya juu. Kutokana na kufungwa kwa shule takribani ya wanafunzi wa elimu ya msingi (basic education) 13,544,069 na wanafunzi wa sekondari 2,023,205 wote walikuwa nyumbani (BEMIS 2019). Katika kipindi cha takribani miezi mitatu ya wanafunzi kufunga shule, serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo (Development Partners) na mashirika yasiyo ya kiserikali wamefanikisha kurusha vipindi radioni na televisheni kuhakikisha mwanafunzi anaendelea kusoma kipindi cha COVID-19. Aidha zipo changamoto zilizojitokeza kipindi cha kufungwa kwa shule ikiwemo:

  1. Sio kila mtoto wa Kitanzania alipata fursa ya kusoma akiwa nyumbani hasa wanafunzi wanaoishi  katika mazingira magumu na hawana televisheni, radio na simu janja (smartphone) zakuwa saidia kujifunza kipindi wapo nyumbani. Kundi lingine ni  watoto wenye mahitaji maalumu  mfano, wasioona,viziwi, nk.
  2. Mtoto wa kike amekuwa hatarini zaidi kipindi cha kufungwa kwa shule kwani amekuwa akipitia changamoto nyingi mfano, kufanya kazi nyingi nyumbani na kukosa muda wa kujisomea, kuwindwa na watu wasio na nia nzuri(mafataki), kiujumla ulinzi wa jamii kwa mtoto wa kike (social protection) umekuwa changamoto. Takwimu za mkoa wa Shinyanga zinaonyesha kuwa kwa kipindi cha mwezi Machi na Aprili 2020 watoto wa kike wenye umri wa miaka 13-17 kati yao 102 wamepata ujauzito katika kipindi hiki cha likizo ya corona (Shinyanga regional reports).

WANAFUNZI KUREJEA SHULENI

Tunaipongeza serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wa kuwarejesha watoto shuleni kama ilivyo tamkwa na Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli, nanukuu ”Kutokana na kushuka kwa hali ya maambukizi ya ugonjwa wa corona napenda kutumia nafasi hii kutangaza kuwa shule zote zilizokuwa zimebaki zifunguliwe, lakini pia shughuli zote zilizokuwa zimezuiwa nazo ziendelee”. Mwisho wa kunukuu. Baada ya kutoa tamko hilo, Rais Magufuli aliwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari ili kuepukana na maambukizi ya virusi vya corona.

Yamkini wazazi na wadau wa elimu wamekuwa wakijiuliza kama shule zetu zipo salama vyakutosha kuwalinda watoto wakirudi shuleni wasipate maambukizi ya virusi vya corona ukizingatia baadhi ya mazingira ya shule yalitumika kama sehemu za karantini kwa wagonjwa wenye dalili za virusi vya corona. Lakini pia baadhi ya shule zina idadi kubwa ya wanafunzi darasani.

Kulingana na muongozo uliotolewa na wizara ya afya, tumehakikishiwa kuwa shule zetu zimefanyiwa maboresho ya kiafya ili kuhakikisha afya ya mwanafunzi arudipo shuleni inakuwa kwenye usalama. Maboresho haya ya afya yamejumuisha kutakasa mazingira yote ya shule, uwepo wa vifaa vya kunawia mikono nk.

Sisi kama Mtandao wa Elimu Tanzania tulichukua hatua ya kuwakutanisha viongozi wa serikali (TAMISEMI na MoEST), washirika wa maendeleo (Development Partners) na wadau wengine wa elimu kujadiliana miundombinu wezeshi itakayo hakikisha afya ya mwanafunzi atakapo rudi shuleni ni salama. Japokuwa tulikutana na baadhi ya changamoto kwa wanafunzi wa vyuo kutofuata taratibu za afya kama ilivyotolewa na wizara ya afya. Hivyobasi Mtandao unapenda kuchukua fursa hii kuwasihi wanafunzi waliokwisha fungua shule na wanaotarajia kufungua shule kufuata miongozo yote ya wizara ya afya kama unawaji wa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni, uvaaji wa barakoa, kukaa kwa nafasi nk lengo likiwa ni kudhibiti maambukizi ya COVID-19.

 USHAURI KWA SERIKALI

Aidha Mtandao unapenda kuchukua nafasi hii kuipongeza serikali kwa kuchukua hatua zote muhimu ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona na pia kutambua mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuendelea kuyashirikisha katika majadiliano na maamuzi yanayoleta maendeleo katika sekta ya elimu. Pili, Mtandao unapenda kuiomba serikali kuboresha maeneo makuu matano (5) yatakayoleta chachu ya kudumu katika maendeleo ya sekta ya elimu;

  1. Kuendelea kutakasa mazingira ya shule mara kwa mara ili kuthibiti maambukizi ya virusi vya corona na magonjwa mengine kwa ujumla.
  2. Kukuza huduma ya mwongozo na ushauri (guidance and counselling services) katika shule ili kuhakikisha wanafunzi na walimu wanamaandalizi bora ya afya ya kiakili.
  3. Kuweka mkazo katika kukuza matumizi ya TEHAMA katika kufundisha na kujifunzia.
  4. Kuboresha vituo vya elimu ya njia mbadala (alternative education pathways) kutokana na ongezeko la uhitaji wa wanafunzi kupata elimu kupitia njia hizi mfano VETA nk. Kama mlivyoninukuu hapo awali katika mkoa wa Shinyanga watoto wa kike102 walipata mimba kipindi cha corona, na hivyo hawatoruhusiwa kuendelea na mfumo rasmi wa elimu kama sheria zinavyoelekeza.
  5. Kutoa elimu endelevu kwa jamii kuhusiana na ulinzi wa mtoto dhidi ya maambukizi ya corona na hata magonjwa mengine. Mtandao unapenda kutoa rai kwa jamii kwa ujumla kuwajibika kuwalinda watoto wote.

HITIMISHO

Mwisho mtandao unapenda kuwashukuru waandishi wote wa habari mlioitikia wito na kufika katika ofisi za TEN/MET na kusikiliza maoni yetu kulingana na ufunguzi wa shule mnamo Jumatatu ya tarehe 29 Juni 2020. Nawasihi tuzidi kushirikiana kuhakikisha tunapata ufumbuzi wa changamoto zote zilizojitokeza kutokana na virusi vya corona vilivyo athiri maendeleo ya sekta ya elimu na jamii kiujumla.

Asanteni sana na mbarikiwe

Imetolewa na TEN/MET

Tafadhali pakua hapa