Wito unatolewa kwa  jamii nzima kukabili na kutokomeza ukatili dhidi ya watoto nchini. Kila Mtanzania, mzazi/mlezi, mwalimu na jamii nzima kwa ujumla wetu tunawajibu wa kukemea vitendo na viashiria vya  ukatili dhidi ya  watoto katika eneo na mazingira mahalia. Bila kujali nafasi zetu, jamii nzima tunao  wajibu wa kuchukua hatua sitahiki inapotokea vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto vinafanywa mbele yetu au tupatapotaarifa sahihi zinazohusu ukatili dhidi ya mtoto.

Tunaukumbusha umma wa watanzania kuwa, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ni jambo changamano, kwani hufanyika katika muktadha na nyanja nyingi katika kila nchi duniani kwa dhana ya kuwarekebisha kimaadili. Njia na dhana hii ni potofu kwani mtoto hawezi kurekebishwa na  kujengwa katika maadili mema kwa njia ya ukatili badala yake ukatili huu umwathiri zaidi kisaikolojia na kuharibu jitihada za kufikia malengo yake. Kwa hivyo, vitendo vya ukatili dhidi ya mtoto si jambo la kuvumilika  na linahitaji juhudi madhubuti na za makusudi katika kuvikabili na kuvitokomeza vitendo vya kikatili dhidi ya watoto hapa nchini na duniani kote kwa ujumla. Ili kufanikisha adhima hii, tunatoa wito kwa serikali yetu sikivu, jamii ya watanzania na wadau wote  kushirikiana katika kushughulikia matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambayo yanaendelea kushamiri kwa kasi kubwa hapa nchini na duniani kote kama tunavyoshuhudia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. Aidha, tunatoa wito kwa serikali yetu sikivu, kwa kushirikiana na wadau, ifanye mapitio upya  ya sheria na miongozo ya haki na ulinzi wa mtoto ili kuondoa mianya yote inayoweza kutumiwa vibaya na watu waliopewa dhamani ya kuwalea, kuwafundisha na kuwaongoza watoto.

Soma zaidi hapa