Rais wa Tanzania, John Magufuli ameelekeza shule zote zilizokuwa zimefungwa kutokana na janga la corona zifunguliwe kuanzia Juni 29, 2020.
Akitoa agizo hilo katika hotuba yake ya kufunga Bunge la 11, Rais ameelekeza pia kurejea tena kwa shughuli nyingine zilizokuwa zimezuiwa kama watu kufunga ndoa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19).
Serikali ilichukua hatua ya kufunga shule zote na taasisi nyingine za elimu pamoja na kuzuia shughuli zinazohusisha mikusanyiko ya watu mapema Machi mwaka huu, kufuatia kuripotiwa kwa muathirika wa kwanza wa corona nchini Machi 15, 2020.
Kufunguliwa kwa shule kumekuja ikiwa ni wiki mbili tangu vyuo vya elimu ya juu vilipofunguliwa pamoja na wanafunzi wa kidato cha sita kurejea masomoni kwa ajili ya kujiandaa na mitihani ya kuhitimu elimu ya sekondari.
source: www.tbc.go.tz